Na Benny Mwaipaja, Dodoma
 
SERIKALI imewahakikishia watanzania kuwa uwekezaji mpya wa zaidi ya dola za Marekani milioni 400 utakaofanywa na Kiwanda cha Saruji cha Twiga kwenye Kiwanda cha Saruji Tanga, utaongeza uzalishaji wa saruji, kukuza ajira na mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali.
 
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), walipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda cha Tanga Cement, Jijini Dodoma.
 
Dkt. Kijaji alisema kuwa Kiwanda cha Saruji cha Tanga kupata mwekezaji mpya lilikuwa jambo lisilokwepeka kutokana kiwanda hicho kupata hasara kwenye mizania yake ya biashara kwa miaka mitano mfululizo na hivyo kuweka rehani zaidi za ajira za wafanyakazi 3,000 wa kiwanda hicho pamoja na mapato ya Serikali.
 
Alisema kuwa mtaji huo wa dola za Marekani milioni 400, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 930, utakifanya kiwanda hicho kuzalisha saruji kwa wingi itakayokidhi soko la ndani, Afrika Mashariki, na Eneo Huru la Biashara la Afrika kwa ujumla.
 
“Tunaamini kuwa Kiwanda cha Tanga Cement kitaongeza uzalishaji kwa kiwango chake cha mwanzo na kuendelea kutoa ajira za watanzania 3,000, pamoja na matarajio ya kiwanda hicho kuanza kulipa kodi Serikalini baada ya mwaka mmoja ujao” alisema Dkt. Kijaji
 
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alisema kuwa uamuzi wa Serikali wa kukinusuru kiwanda hicho umechukuliwa kwa umakini mkubwa na kuishauri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuharakisha uwekezaji huo ili ukamilike kama ilivyopangwa.
 
Alisema kiwanda hicho kina mchango mkubwa wa kukuza ajira, kutoa kodi Serikalini lakini kikubwa ni kuongezeka kwa uzalishaji wa saruji kunakotarajiwa ambako kutawafanya wananchi wapate saruji kwa bei nafuu ili kujenga makazi bora.
 
“Uzalishaji ufanyike ili wananchi wapate saruji ili wajenge nyumba bora, na watafanya hivyo bei ya saruji ikiwa chini, uzalishaji ukiwa mkubwa, tunauhakika wananchi watapata sementi kwa bei nafuu” alisema Dkt. Nchemba.
 
Aliwaomba Tanga Cement kuwafikishia wawekezaji wengine taarifa za uwepo wa mazingira bora ya uwekezaji hapa nchini na kuwaomba na wao pia wachangamkie fursa hizo ili waweze kunufaika kibiashara.
 
Aliitaka timu ya wataalam wa Wizara ya Fedha na Mipango, Tanga Cement na mwekezaji mpya Twiga Cement, kukamilisha haraka ukokotoaji wa hesabu za kodi ya zuio (Capital gain tax) ambayo Serikali inatakiwa kupata kutokana na uwekezaji huo.
 
Kwa uopande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho cha Saruji Tanga Bw. Reihardt Swart, aliipongeza Serikali kwa kukamilisha mchakato huo wa kuiwezesha kampuni yake kukabidhi kiwanda chao kwa mwekezaji mwingine-Twaga Cement, ahatua ambayo alisema itaongeza mchango wa kiwanda katika uchumi wa nchi.
 
 
Kwa mujibu wa Dkt. Kijaji, Tanga Cement, inatarajia kuachia hisa zake asilimia 68.33 kwa Kampuni ya Twiga Cement ili iwekeze mtaji huo wa zaidi ya dola za Marekani milioni 400 kwa ajili ya kuzalisha saruji itakayosaidia kupunguza upungufu wa bidhaa hiyo nchini.
 
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma) 
Share Story

Facebook Comments