Na Farida Ramadhani-Dodoma

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewaagiza wataalamu wa Wizara ya Fedha na Mipango na ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kujadili namna ya kushughulikia athari za upungufu wa dola za Kimarekani katika mzunguko wa fedha ili kunusuru uchumi wa nchi zinazoendelea.

Mhe. Dkt. Nchemba (Mb) ametoa maagizo hayo wakati wa kufungua kikao kilichowashirikisha wataalam kutoka Shirika la Fedha na Kimataifa (IMF) waliowasili nchini kwa ajili ya kufanya tathimini ya Program ya Huduma za Mikopo (EFC), kwa kushirikiana na wataalam wa ndani wa Serikali.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akimsikiliza Kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Harris Tsangaride wakati wa kikao cha wataalamu wa Wizara hiyo na IMF, waliokuja nchini kufanya tathmini ya Program ya Huduma za Mikopo (EFC), jijini Dodoma.

Alisema mabadiliko ya Sera za Fedha nchini Marekani ya kubana matumzi na kupunguza dola kwenye mzunguko wa fedha, yameleta athari zinazoonekana mpaka kwenye nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
“Tumekuwa tukirejea Uviko na vita baina ya Urusi na Ukraini kama moja ya vitu vinavyoathiri uchumi wa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania lakini upungufu wa dola unaathiri uchumi kwa kiwango kikubwa ikiwemo uagizaji wa mafuta na uagizwaji wa bidhaa mbalimbali zinazotumika katika shughuli za Sekta Binafsi”, alisema Dkt. Nchemba.

Alisema ni vema kutafuta namna ya kushughulikia jambo hilo kisera ili kunusuru nchi zinazoendelea kwa kuwa sekta ya nje ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.

Kwa upande wake Kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Harris Tsangaride, alisema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Tanzania ili kuhakikisha nchi inaendelea kupiga hatua kiuchumi na kijamii.
Aliipongeza Serikali kwa Sera zake nzuri ambazo zinaendelea kutekelezwa katika kukabiliana na athari za vita ya Ukraine na kuongeza kuwa ni matarajio yao kuwa zitaendelea kuchokea ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi.

Bw. Tsangaride alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache katika kanda ambazo zinafanya vizuri katika kutekeleza programu mbalimbali kwa kushirikiana na Shirika hilo na hivyo katika kikao hicho watajadiliana namna bora ya kuendelea kuiona nchi ikifanya vizuri zaidi.

Mwisho.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), Bw. Harris Tsangaride baada ya kufungua kikao cha wataalamu wa Wizara hiyo na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), waliofika nchini kwa ajili ya kufanya tathmini ya Program ya Huduma za Mikopo (EFC), jijini Dodoma.
Share Story

Facebook Comments