Waziri wa Fedha na Mipango Mhe Dkt Mwigulu Nchemba (MB), ameongoza harambee ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kati (Singida), juu ya ujenzi wa shule mbili za sekondari, zinazotarajiwa kugharimu Sh. Milioni 500/=
Kwa mujibu, Dayosisi hiyo itajenga shule hizo moja katika manispaa ya Singida, kwenye eneo la misioni lililopo Kititimo na ile ya pili itajengwa makao makuu ya wilaya ya Iramba mjini Kiomboi.
Akizungumza na waumini wa Kanisa hilo wakati wa Ibada hiyo maalumu iliyofanyika kwenye Usharika wa Emmanuel, ambao ni makao makuu ya Dayosisi hiyo Singida Mjini, Waziri Dkt. Nchemba alisema kuwa, serikali inaunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Taasisi mbalimbali za dini, ikiwemo dhehebu la Kilutheri, ambalo limeshiriki vyema kuweka miundombinu ya elimu na afya.
Dk. Nchemba alifafanua kuwa, muundo wa shughuli za maendeleo kati ya Kanisa na serikali, umekuwa kwenye hali ya kuridhisha na kuleta mafanikio ya dhati katika mageuzi ya kiuchumi.
Aidha Dkk Nchemba ameitaka jamii kuwekeza kwenye shughuli za kilimo ili sekta hiyo iweze kuleta tija nchini, hasa kupitia kundi la vijana ambalo hivi sasa linapoteza mwelekeo pamoja na serikali kugharamia masomo yao hadi ngazi ya elimu ya juu.
Kwa upande wake Askofu wa Dayosisi ya mashariki na Pwani Dkt. Alex Malasusa aliyeshiriki kwenye harambee hiyo, wakati akitoa neno la mahubiri, aliwataka Wakristo kujenga utamaduni wa kumtolea sadaka mwenyezi Mungu ili baadaye wapate baraka na hivyo kufanikiwa katika maisha yao.
Pia Dkt. Malasusa aliwataka Wakristo na Watanzania kwa ujumla, kuendelea kulipa kodi kwa mamlaka husima, ili kuipa serikali uwezo wa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi kwenye harambee hiyo, askofu wa KKKT Dayosisi ya Kati, Dkt Syprian Hillinti, alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kulirejeshea Kanisa hilo shule ya sekondari Ruruma iliyopo wilayani Iramba, ambayo hivi sasa ipo chini ya Jumuiya ya wazazi ya Chama Cha Mapinduzi.
Awali shule hiyo miaka ya nyuma ilimilikiwa na Kanisa hilo, lakini ikaikabidhi serikali, na sasa kanisa linaiomba ili iweze kuendelezwa kutokana na historia yake nzuri ya eneo hilo kuwa kitovu cha injili kwa dhehebu hilo.
Katika harambee hiyo, jumla ya TZS 443,063,800/= zilikusanywa, huku mgeni rasmi Dkt. Mwigulu Nchemba akichangia TZS Milioni 5.
Baadhi ya wabunge walioongozana na Waziri Dkt Mwigulu Nchemba ni mbunge wa Makete Festo Sanga (Makete Njombe), Mussa Sima (Singida mjini), Miraji Mtaturu (Singida mashariki), Ruben Kwagila (Handeni Tanga) na Anna Lupembe (Nsimbo Mpanda)
Facebook Comments