Na. Peter Haule, WFM, Dodoma

Bunge limepitisha Muswada wa marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa mwaka 2023 ambayo itawasilishwa kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili isainiwe na kuwa Sheria kamili.

Akizungumza wakati wa kuwasilisha mswada huo bungeni, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alisema kuwa lengo la marekebisho yaliyopendekezwa katika Mswada huo lilikuwa kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa baadhi ya masharti yaliyomo katika Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sura 103.

“Masharti yaliyokuwemo yalisababisha kuwepo kwa ushiriki hafifu wa Sekta Binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa utaratibu wa ubia”, alisema Dkt. Nchemba

Dkt. Nchemba alisema kuwa changamoto zilizojitokeza ni pamoja na Sheria kutotoa haki kwa wabia kutoka Sekta Binafsi kuwasilisha migogoro kwenye mahakama za kimataifa kwa utatuzi, kutoainisha aina ya misaada ya kifedha (public funding) itakayoidhinishwa kupitia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada

Alibainisha changamoto nyingine kuwa ni pamoja na Sheria kutoruhusu Mamlaka za Serikali kufanya ununuzi wa moja kwa moja wa mbia kutoka Sekta Binafsi kwa ajili ya kutekeleza miradi inayoibuliwa na mamlaka hizo na  kutoweka masharti kwa Mwekezaji kutoka Sekta Binafsi aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa PPP kuunda Kampuni.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Mswada huo unakusudia kurekebisha Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sura 103 ili pamoja na mambo mengine kuiwezesha Sekta Binafsi kushiriki kikamilifu katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa utaratibu wa PPP.

Pia marekebisho hayo yanalenga kuimarika kwa huduma za jamii kutokana na ubunifu, teknolojia na ujuzi kutoka Sekta Binafsi na pia kupungua kwa muda wa maandalizi ya miradi na hivyo kuharakisha utekelezaji wa  miradi ya PPP.

Alisema kuwa Mswada huo umezingatia kwa kiasi kikubwa ushauri na mapendekezo mazuri ya Kamati na wadau mbalimbali kwa ujumla ambao kwa nyakati tofauti walitoa ushauri wao.

Aidha, amemshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wataalam wake, wataalam wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuandaa Mswada huo pamoja na marekebisho yake.

Share Story

Facebook Comments