Na. Peter Haule, WFM, Dodoma

Benki ya Standard Chartered ipo katika hatua za mwisho za utaratibu wa kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa vipande vilivyobakia vya reli ya kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR) ikiwa ni pamoja na kipande cha Makotopora-Tabora, Tabora – Isaka, Isaka-Mwanza na kipande cha kuanzia Tabora hadi Kigoma.

Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa tano kushoto) na ujumbe wa Benki ya Standard Chartered ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered anayesimamia nchi za Afrika na Mashariki ya Kati, Bw. Sunil Kaushal, ukiwa katika picha ya pamoja baada ya Mkutano kati yao uliofanyika jijini Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered anayesimamia nchi za Afrika na Mashariki ya Kati, Bw. Sunil Kaushal.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania na Benki ya Standard Chartered, imekuwa na ushirikiano mzuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya reli ambayo inaendelea vizuri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered anayesimamia nchi za Afrika na Mashariki ya Kati, Bw. Sunil Kaushal Benki ya Standard Chartered, akieleza kufikiwa kwa hatua za mwisho za upatikanaji wa fedha za ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), jijini Dodoma.

“Tumekuwa na majadiliano kuhusu vipande vya reli ambavyo taratibu za kupata fedha zilikuwa hazijakamilika kikiwemo kipande cha Makotopora-Tabora, Tabora – Isaka, Isaka-Mwanza na kipande cha kuanzia Tabora hadi Kigoma”, alisema Dkt. Nchemba

Dkt. Nchemba alimshukuru Mkurugenzi huyo na timu yake kwa ujumbe waliouleta ambao unaeleza kuwa Benki hiyo ipo kwenye hatua za mwisho za taratibu za kupata fedha kwa ajili ya vipande hivyo vya Reli

Alisema kuwa Reli ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na mara zote amekuwa akiuliza upatikanaji wa fedha umefikia hatua gani

Alisema kuwa kwa sasa anayofuraha kumpelekea ujumbe, Mhe. Rais kuwa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vipande hivyo umefikia hatua nzuri.

Ujumbe kutoka Benki ya Standard Chartered ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered anayesimamia nchi za Afrika na Mashariki ya Kati, Bw. Sunil Kaushal Benki ya Standard Chartered (kulia) ukifuatilia maelezo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani) kuhusu upatikanaji wa fedha za kujenga vipande vya reli ambavyo havijakamilika.

Dkt. Nchemba ameziagiza timu za wataalam zinazoshughulikia jambo hilo kuhakikisha zinafanya taratibu za ukamilishaji wa upatikanaji wa fedha hizo ili miradi iende kwa kasi ambayo watanzania wanaitarajia.

Aidha ameipongeza timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kwa kukamilisha masuala mbalimbali yaliyokuwa yamejitokeza likiwemo suala la mazingira ambalo limepatiwa ufumbuzi

Dkt Nchemba alisema kuwa ni vema kumaliza suala hilo la ujenzi ili kuendelea na fursa za miradi mingine ambayo itafungua fursa si tu Tanzania lakini pia katika nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered anayesimamia nchi za Afrika na Mashariki ya Kati, Bw. Sunil Kaushal, alisema kuwa Tanzania inafanya juhudi kubwa katika kusimamia uchumi na pia inafursa nyingi za uwekezaji ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika zikiwemo za Afrika Mashariki na kwamba Benki yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akielezea umuhimu wa Reli ya Kisasa wakati wa mkutano kati yake na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered anayesimamia nchi za Afrika na Mashariki ya Kati, Bw. Sunil Kaushal (hayupo pichani), jijini Dodoma.
Share Story

Facebook Comments