Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
 
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewataka Wakala wa Barabara nchini -TANROADS kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa Mkandarasi atakayejenga Daraja la Mto Msimbazi ili kuwaondolea wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, changamoto ya mafuriko.
 
Dkt. Nchemba ametoa kauli hiyo baada ya kuongoza Ujumbe wa Serikali na Benki ya Dunia kutembelea eneo la Jangwani ambapo mradi wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, unatarajiwa kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa daraja kubwa la juu la Jangwani, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mapema mwakani, kwa gharama ya zaidi ya dola za marekani milioni 350. 
 
“Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametuelekeza tufanye kikao na Benki ya Dunia ili mradi huu wa daraja na ujenzi wa barabara za Jiji la Dar es Salaam, uanze kutekelezwa haraka ili kuwaondolea wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kero ya mafuriko pamoja na kuimarisha mipango miji” Alisema Dkt. Nchemba.
Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (wa saba kulia), Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deo Ndejembi (wa tisa kushoto), Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila (wa sita kulia), Naibu Spika na Mbunge wa Ilala, Mhe. Mussa Azzan Zungu (wa nane kulia), Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete (wa tisa kulia), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, pamoja na wataalamu kutoka Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ziara fupi ya kutembelea eneo la jangwani ambapo, Mradi mkubwa wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, ikiwemo ujenzi wa daraja kubwa la juu la Jangwani, utajengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mapema mwakani, kwa gharama ya zaidi ya dola za marekani milioni 350. Lengo la mradi huo ni kukabiliana na mafuriko pamoja na kuimarisha mipango miji. Ziara hiyo fupi imefanyika baada ya kikao kati ya Serikali na Benki ya Dunia, kilichofanyika ofisi za Hazina Ndogo, Dar es Salaam.
  
Alisema kuwa Jiji la Dar es Salaam ni kitovu cha biashara na linategemewa na nchi zaidi ya nane zinazopakana na Tanzania na kwamba kukamilika kwa miradi hiyo ya daraja na barabara za Jiji hilo zitachochea shughuli za kiuchumi.
 
“Wizara ya Fedha kupitia Benki ya Dunia tunawahakikishia kuwa fedha zipo kinachotakiwa ni kuanza kwa utekelezaji ili kutekeleza maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” Alisisitiza Dkt. Nchemba.
 
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Deo Ndejembi, ambao ndio watekelezaji wa mradi huo, wameahidi kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi ili thamani ya fedha itakayotumika ilingane na ubora wa mradi.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Albert Chalamila, alihimiza pia kuanza haraka kwa ujenzi wa mradi huo ili kutatua kero za wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na kuzingatia usanifu wa viwango vya juu.
 
“Ujenzi wa barabara na madaraja makubwa kama haya kuna maanisha kuufungua mkoa kiuchumi sasa tusibaki kulumbana na kubishana kwa ajenda ndogo ambazo wakati fulani hazina mashiko kwa mustakabali wa Taifa letu, lakini pia ile maana halisi ya Mkoa wa Dar es Salaam kuwa Jiji la kibiashara iweze kuonekana kwa miundombinu hii” alisema Bw. Chalamila.
 
Naye Mbunge wa Ilala Mussa Azzan Zungu, alisema kuwa Serikali inaboresha Bandari ya Dar es Salaam kwa kumpata mwekezaji DP World ambapo mizigo mingi itakayopokelewa, mizigo ambayo inahitaji barabara bora ili kuharakisha uondoshaji na usafirishaji wa mizigo kwenye nchini na nchi Jirani ambapo nchi inatarajia kupata zaidi ya shilingi trilioni 26 kwa mwaka kutokana na uwekezaji huo, fedha ambazo zitachangia maendeleo ya nchi.
 
“Kama mnavyofahamu, Jiji la Dar es Salaam linachangia asilimia 85 ya pato la Taifa na kwamba kukamilika kwa mradi huu kutachangia upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya Taifa” alisema Mhe. Zungu
 
Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete, alisema kuwa Benki yake itatoa mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni 350 ili miradi hiyo itakayotekelezwa Jijini Dar es Salaam iweze kuchangia maendeleo ya nchi kwa kupanga mji, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuboresha miundombinu ya usafiri na kudhibiti taka ngumu.
 
Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (wa saba kulia), Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deo Ndejembi (wa tisa kushoto), Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila (wa sita kulia), Naibu Spika na Mbunge wa Ilala, Mhe. Mussa Azzan Zungu (wa nane kulia), Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete (wa tisa kulia), Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, pamoja na wataalamu kutoka Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ziara fupi ya kutembelea eneo la jangwani ambapo, Mradi mkubwa wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, ikiwemo ujenzi wa daraja kubwa la juu la Jangwani, utajengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia mapema mwakani, kwa gharama ya zaidi ya dola za marekani milioni 350. Lengo la mradi huo ni kukabiliana na mafuriko pamoja na kuimarisha mipango miji. Ziara hiyo fupi imefanyika baada ya kikao kati ya Serikali na Benki ya Dunia, kilichofanyika ofisi za Hazina Ndogo, Dar es Salaam.
Baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wamepongeza hatua ya Serikali ya kuweka miundombinu imara ya jiji hilo itakayosaidia kuwaondolea kero ya foleni na mafuriko wakati wa mvua zinaponyesha.
 
Walisema kuwa wamekuwa wakipoteza muda na mali zao wakati wa mafuriko na kwamba ujenzi wa daraja hilo kubwa na refu litakaloanzia Magomeni hadi Fire, utakuwa mwarobaini wa matatizo yao na kummwagia sifa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulivalia njuga suala hilo.
 
Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi (DMDP II) utatumia fedha hizo za Serikali na mkpo kutoka Benki ya Dunia kujenga miundombinu ya barabara, mifereji, maeneo ya wazi, masoko, vituo vya mabasi, na kurekebisha miundombinu ya taka ngumumiundombinu ya usafiri, mabadiliko ya tabia nchi kwa jiji la Dar es Salaam zinazosababisha mafuriko na kudhibiti taka ngumu
Share Story

Facebook Comments