Serikali imeeleza kuwa imeweka ukomo wa bei za bidhaa ambazo Serikali inanunua kwa kuzingatia bei za soko ili kudhibiti ununuzi wa bidhaa hizo kwa gharama kubwa kuliko zilizopo Sokoni.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Asia Abdulkarim Halamga, aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu kushusha gharama za ununuzi na kuagiza bidhaa hususani magari kulingana na bei ya Soko.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali imeweka msisitizo katika Sheria ya manunuzi kwa kuweka ukomo wa bei za bidhaa ambazo Serikali inafanya manunuzi kwa kuzingatia bei za soko.

“Ukomo wa bei za manunuzi ambayo Serikali inafanya si tu kwa magari lakini pia kwa bidhaa nyingine, kuanzia mfumo wenyewe wa manunuzi ambapo Afisa Masuuli anapotaka kulipa kwa gharama za juu kuliko bei ya soko inayotambulika atakuwa amekiuka Sheria”, alisema Dkt. Nchemba.

Akizungumzia suala la kuagiza bidhaa moja kwa moja kutoka viwandani bila kupitia kwa Wakala, Dkt. Nchemba alisema kuwa kuna baadhi ya mazingira yakiwemo ya viwango vya ubora vya baadhi ya bidhaa, Sheria inamruhusu Afisa Manunuzi kununua moja kwa moja lakini hutokea kwa baadhi ya maeneo wanunuzi wenyewe hawapendi Taasisi nunuzi kwenda moja kwa moja kiwandani kwa kuwa viwanda hivyo vinaushirikiano wa moja kwa moja kwa wale wanaofanya nao biashara ambao ni matawi yao au mawakala.

Hata hivyo alisema kuwa mtazamo wa Serikali ni kuendelea kupunguza matumizi ya magari ambapo Serikali iliweka utaratibu kwa wale wenye sifa ya kuwa na magari wakopeshwe ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kuyaendesha na kuyafanyia huduma za matengenezo.

Kuhusu Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) kuchelewesha ununuzi wa magari ya Serikali, Dkt. Nchemba alisema kuwa ucheleweshaji huo ulisababishwa na Mabadiliko ya aina (models) za magari yanayotumiwa na Serikali ambapo upatikanaji wa aina mpya huweza kuchukua muda mrefu zaidi kutegemea na idadi ya mahitaji kwa Serikali.

Alieleza kuwa sababu nyingine ni athari za kiuchumi zinazoathiri mnyororo wa uzalishaji na usafirishaji mfano UVIKO-19, iliyosababisha viwanda vinavyozalisha vipuri vya magari kufungwa na kusababisha changamoto ya uhaba wa vifaa vya TEHAMA ambavyo kwa sehemu kubwa ya magari ya kisasa hutumia teknolojia kubwa ya umeme na changamoto ya usafirishaji wa magari, ikiwemo uhaba wa wasafirishaji na ukosefu wa makasha ya kusafirisha mizigo.

Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba, alisema kuwa, kwa sasa mnyororo wa ununuzi wa magari duniani umeanza kuimarika na magari yote yanafika kwa wakati na kukabidhiwa kwa Taasisi zilizoagiza, hivyo upatikanaji wa magari kwa wakati umerejea

Share Story

Facebook Comments