Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) ameiagiza Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za kodi (TOST) kuhakikisha inatatua migogoro mbalimbali ya kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kukusanya mapato pamoja na kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.
Dkt. Nchemba alitoa agizo hilo Jijini Dodoma wakati akizindua rasmi Ofisi hiyo mpya ambayo iko chini ya Wizara ya Fedha.
Mhe. Nchemba alisema kuwa Serikali inatarajia kwamba Ofisi hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya kikodi na kuongeza kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari, hivyo kuongeza mapato ya Serikali.
“Ofisi hii utasaidie kupunguza migogoro ya kodi na kuongeza kiwango cha ulipaji kodi kwa hiari, siku tukifanikiwa kuongeza idadi ya walipakodi (taxbase), tutakuwa na uhuru mkubwa sana wa kupunguza hivi viwango vya ulipaji kodi”, alisema Mhe. Dkt. Nchemba.
Alisema ni matarajio ya Serikali kuwa ustawi wa biashara utaongezeka kutokana na walipa kodi kupata jukwaa huru litakalotoa fursa ya kusikiliza changamoto zinazohusu usimamizi wa sheria ya kodi pamoja na huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mhe. Dkt. Alisema Wizara ya Fedha itaendelea kusimamia na kuboresha utendaji wa Taasisi hiyo kwa kuhakikisha kuwa mahitaji yote muhimu yanapatikana ikiwemo rasilimali watu, vifaa na mifumo ya kisasa ili iweze kutoa huduma bora kwa walipa kodi.
Aidha, Aliagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kukusanya kodi kwa weledi kwa kutafuta njia ya majadiliano na wafanyabiashara wanaokiuka taratibu badala ya kufunga biashara zao.
Mhe. Dkt. Nchemba aliwaagiza Wafanayabiashara kufanya biashara zao kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizopo ili kuepusha misuguano isiyo ya lazima na Mamlaka ya Mapato.
Pia alitoa rai kwa wananchi kuwa wazalendo kwa kulipa kodi stahiki na kwa wakati, kudai risiti halali kulingana na kiwango cha fedha walichotoa na wafanyabiashara kufanya matumizi sahihi ya mshine za kutolea risiti kwa njia ya kielekroniki (EFDs) pamoja na kutoa risti halali kwa wateja wao.
“Watu wanaostahili kutumia mashine za EFDs watumie, kutokufanya hivyo ni kujitafutia matatizo wenyewe. Kutokutoa risiti na kusingizia mifumo sio suluhisho la kudumu, huku ni kuahirisha matatizo” alisitiza Mhe. Dkt. Nchemba.
Alisema kufanya hivyo, kutaiwezesha Serikali kutoa huduma muhimu za kijamii ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali itakayoboresha maisha yao na kupunguza umasikini ikiwemo maji, elimu, miundombinu wezeshi kiuchumi na mambo mengine mengi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Usuhulishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Bw. Robert Manyama alisema kuwa Taasisi yake imejipanga kutatua changamoto za taarifa za kikodi za wananchi katika ubora wa hali ya juu kwa kuwa imeweka mazingira rafiki na rahisi ya wananchi kuwasilisha malalamiko yao popote walipo pamoja na kuwa na wafanyakazi wenye ueledi na waliotayari kutoa huduma kwa walipa kodi.
“Kipaumbele cha Ofisi hii ni kuhakikisha kwamba malalamiko yote yanashughulikiwa kwa uhuru kamili, haraka, haki na usawa”, alibainisha.
Alisema Ofisi hiyo imeanzishwa kutokana na marekebisho ya Sheria ya Fedha namba 8 ya mwaka 2019, yaliyosababisha marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi SURA 438, kwa kuongeza sehemu ya IIIA – Uanzishaji wa Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (Establishment of Tax Ombudsman office.)
Bw. Manyama alisema marekebisho ya sheria yaliipatia Ofisi hiyo jukumu mahususi la kupokea, kusajili na kusuluhisha Malalamiko yatokanayo na usimamizi wa sheria za kodi ili kuyapunguza na kutoa mapendekezo ya maboresho ya mfumo wa ukusanyaji kodi nchini pamoja na kuongeza ulipaji kodi wa hiari na kupunguza gharama za ukusanyaji wa kodi ya Serikali.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Daniel Baran Sillo (Mb), alisema Kamati hiyo imependekeza Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi kuhakikisha inajulikana kwa wadau wote wa kodi nchini na itekeleze majukumu yake kikamilifu ya kutatua changamoto za walipakodi.
Alisema Kamati pia imependekeza Ofisi hiyo kuendelea kushauri namna ya kutatua changamo ya mifumo ya kodi nchini iliyosababisha migogoro na kuifanyia marekebisho mifumo husika.
Mhe. Sillo aliishauri Ofisi hiyo iendelee kufanyia kazi changamoto za kikodi zinazojirudia na kutafuta suluhisho la kudumu huku akitolea mfano wa tatizo la utoaji na uombaji risiti.
Aidha, Kamati ilipendekeza Serikali, kupitia Taasisi hiyo, itafute mfumo wa kielektroniki utakaotumika kupokea malalamiko, kuyashughulikia na kutoa mrejesho huku kwa wadau na kusisitiza kuwepo uwazi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Facebook Comments