Na Benny Mwaipaja, Dodoma
 
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha sera za kodi ili kuchochea uwekezaji kutoka sekta binafsi ili kukuza uchumi wa nchi, ajira na maisha bora kwa watanzania.
 
Dkt. Nchemba (Mb) amesema hayo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, Bw. Philip Besiimire.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), akizungumza wakati wa kikao chake na ujumbe kutoka Kampuni ya Vodacom Tanzania (kulia) ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya hiyo, Bw. Philip Besiimire, jijini Dodoma, ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano na uwekezaji kati ya Serikali na Kampuni hiyo.
 
Alisema kuwa Sekta binafsi inafanya kazi nzuri kwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kukuza sekta hiyo inayotoa ajira kwa watanzania, kuchangia kodi ya Serikali na kwamba na Vodacom ikiwa miongoni mwa walipa kodi wakubwa.
 
“Tunaipongeza Kampuni ya Vodacom kwa kuendelea kuongeza mtandao wenu unaosaidia katika kutoa huduma jumuishi za kifedha kupitia mfumo wa kutuma na kutoa fedha kidigitali”, alieleza Dkt. Nchemba.
 
Akizungumzia maombi yaliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji huyo wa VODACOM-Tanzania, Bw. Philip Besiimire, kuhusu kupunguza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye simu janja (smartphone) ili watu wengi waweze kutumia simu hizo, Dkt. Nchemba alisema kuwa maoni hayo yawasilishwe na kujadiliwa kwenye kamati ya kukusanya maoni ya sera za kodi ili yachakatwe na kupatiwa ufumbuzi.
Ujumbe kutoka Kampuni ya Vodacom Tanzania ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Philip Besiimire (kulia), ukimsikiliza kwa umakini Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), wakati wa kikao chao kilichofanyika jijini Dodoma, ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano na uwekezaji kati ya Serikali na Kampuni hiyo.
 
Hata hivyo alisema uzoefu umeonesha kuwa baada ya Serikali kufanya hivyo miaka ya nyuma, wananchi wa kawaida hawakunufaika na msamaha huo wa kodi badala yake uliwafaidisha wafanyabiashara ambao licha ya kodi ya ongezeko la thamani kuondolewa kwenye simu janja, bei ya simu hizo ziliendelea kuwa juu zaidi.
 
“Serikali iliwahi kutoa nafuu ya kodi kwenye simu janja na kupoteza kodi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 32, fedha ambazo zingeweza kujenga majengo ya madarasa zaidi ya 100 lakini fedha hizo zilikwenda kwa wauzaji wa bidhaa za simu pekee” alisisitiza Dkt. Nchemba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Bw. Philip Besiimire, akizungumza jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na ujumbe wa Kampuni hiyo, jijini Dodoma, ambapo katika kikao hicho wamejadiliana masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano na uwekezaji kati ya Serikali na Kampuni hiyo.
 
Alitoa rai kwa Kampuni za mawasiliano kuunganisha nguvu na kuingiza nchini simu janja ambazo zitaondolewa Kodi ya Ongezezeko la thamani VAT, watakazoziuza kwa bei nafuu ili wananchi wazitumie kwa mawasiliano na masuala mengine ya kuwaingizia kipato ikiwemo masuala jumuishi ya fedha kidigitali.
 
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa VODACOM Tanzania, Bw. Philip Besiimire, aliipongeza Serikali kwa kuondoa kodi na tozo mbalimbali katika sekta ya mawasiliano ikiwemo tozo kwenye miamala ya simu hatua ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa mzunguko wa fedha katika jamii kupitia miamala ya simu.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa kikao chake na ujumbe kutoka Kampuni ya Vodacom Tanzania ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya hiyo, Bw. Philip Besiimire (hayupo pichani), jijini Dodoma, ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano na uwekezaji kati ya Serikali na Kampuni hiyo.
 
Alisema kuwa wakati wa tozo biashara ilishuka kwa asilimia 35 lakini baada ya Serikali kuondoa tozo hizo, biashara ya miamala ya simu imekua kwa asilimia 20 na wanamatumaini kwamba hali hiyo itakuwa bora zaidi siku za usoni huku akibainisha pia kuwa kiwango cha matumizi ya kulipia huduma mbalimbali kidigitali nayo imekua kwa kasi na kwamba kwa kampuni yake pekee, zaidi ya silingi trilioni moja hupita kwenye mzunguko kwa mwezi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia), akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Bw. Philip Besiimire, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Kampuni hiyo, ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Kampuni hiyo.
 
Aliahidi kuwa Kampuni yake itaendelea kutoa mchango mkubwa kwa taifa kupitia huduma zake mbalimbali zikiwemo za kusaidia jamii kupitia mfuko wake wa kuhudumia jamii na kuiomba Serikali kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye simu janja ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kumiliki simu hizo zenye mchango mkubwa katika Maisha na maendeleo yao.
 
Mwisho
Share Story

Facebook Comments