Tanzania na Global Fund zimesaini Mikataba minne ya misaada yenye thamani ya dola za Marekani milioni 606.9 (sawa na zaidi ya sh. trilioni 1.4) kwa ajili ya kupambana na maradhi ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Malaria na Uimarishaji wa mifumo ya afya nchini.

Mikataba hiyo imesainiwa Jijini Dodoma kati ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), na Mkuu wa Global Fund- Afrika, Bw. Linden Morrison.

Mhe. Nchemba alisema msaada kutoka Global Fund umepangwa kutekelezwa kwa miaka mitatu ambapo mpaka sasa Tanzania imepokea misaada kwa vipindi vinne ambavyo ni Julai 2012 – Desemba 2014, Julai 2015 – Desemba 2017, Januari 2018 – Desemba 2022 na Januari 2021 -Desemba 2023.

“Miradi inayotekelezwa kupitia msaada wa Global Fund kwa kipindi cha kuanzia Januari 2024 hadi Desemba 2026 itatekelezwa na Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Wizara ya Fedha inaendelea kuwa Mpokeaji Mkuu wa Sekta ya Umma na Management and Development for Health (MDH) ni Mpokeaji Mkuu wa pili kwa Sekta Binafsi”, alibainisha Mhe. Nchemba.

Aidha, aliishukuru Global Fund kwa kuendelea kuisaidia Tanzania na kubainisha kuwa misaada hiyo inatokana na juhudi mbalimbali anazofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameifanya nchi iaminike Kimataifa.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Mhe.Ummy Mwalimu alisema watatumia fedha hizo kikamilifu katika kuimarisha kinga dhidi ya UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu ambapo asilimia 75 ya fedha hizo wamezielekeza kwenye bidhaa za afya.

“Kwa upande wa UKIMWI tutahakikisha takribani Watanzania milioni 1.7 ambao wanamaambukizi wanapata dawa za kufubaza makali ya UKIMWI au ARV’s kila mwaka”, alisema Mhe. Mwalimu.

Alisema kwa upande wa malaria, fedha hizo zitatumika kuiwezesha Wizara hiyo kuendelea kutoa huduma bure ya kupima Malaria kwakutumia kipimo cha haraka (MRDT) na kutoa dawa za Malaria kwa watu takribani milioni 10 kwa kipindi cha miaka mitatu.

“Nasisitiza kwamba kipimo cha Malaria cha haraka (MRDT) ni bure, dawa mseto ya Malaria pamoja na sindano ya Malaria kali ni bure kwa sababu fedha hizi tulizopata kutoka Global Fund tunakwenda kutumia kununua vifaa vya kupima Malaria pamoja na dawa”, alisisitiza, Mhe. Mwalimu.

Aidha, aliwaagiza Waganga Wakuu wa mikoa na wilaya zote nchini kusimamia maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha huduma hizo zinatolewa bure kwa wananchi.

Alisema katika upande wa Malaria pia watagawa vyandarua vyenye dawa takribani milioni 22.6 kwa makundi mbalimbali hususan akina mama wajawazito na Watoto walio chini ya miaka mitano.

Kwa upande wa mapambano dhidi ya Kifua Kikuu, Mhe. Mwalimu alisema watatumia fedha hizo kwa ajili ya kuhakikisha wanaibua wagonjwa wapya wa ugonjwa huo.

Alisema fedha hizo pia zitatumika kuimarisha mifumo ya afya ambapo Wizara hiyo imepanga kununua vifaa tiba kwa ajili ya vituo vya huduma za afya katika ngazi ya kata.

Naye Mkuu wa Global Fund Afrika, Bw. Linden Morrison, alisema kuwa Tanzania ni nchi ya nne kwa kupata misaada mingi kutoka Mfuko huo pia imekuwa mstari wa mbele katika ukusanyaji na usimamizi wa rasilimali jambo lililosababisha kupewa misaada hiyo.

Alisema msaada uliotolewa ni kwa kipindi cha mwaka 2024 hadi 2026 na inalenga kuboresha mifumo ya maabara, mitungi ya Oksijeni, kuboresha mazingira ya watumishi wa afya na kuimarisha mnyororo wa thamani.

Aidha Bw. Morrison alisema kuwa msaada huo unakwenda sambamba na vipaumbele vya Serikali ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya Afya nchini.

Ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanikisha kusimamia utekelezaji wa

programu iliyoishia Desemba 2023 ambapo ilipata matokeo mazuri ya matumizi ya fedha kutoka mfuko huo katika masuala yakupunguza maambukizi ya HIV, Maralia na kifua kikuu.

Share Story

Facebook Comments