Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kutokana na sera zake nzuri za kifedha na kiuchumi licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Dunia zikiwemo athari za Uviko 19 na mizozo ya kivita inayoendelea maeneo mbalimbali Duniani.

Amesema hayo jijini Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na timu ya watalaam wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika Ofisi za Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa licha ya changamoto za kiuchumi Duniani kote bado Tanzania iliendelea kuimarika ukilinganisha na nchi nyingine zinazoizunguka kutokana na uimara wa sekta ya kilimo, uchukuzi na ujenzi.

Aidha alieleza kuwa Tanzania inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ya nishati ya umeme wa maji wa Julius Nyerere, mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Daraja la Kigongo – Busisi mkoani Mwanza ambayo kukamilika kwake kutachochea maendeleo ya kiuchumi.

Alisema kuwa Tanzania imejielekeza pia katika maendeleo ya viwanda na kupeleka umeme vijijini ambapo takribani vijiji 1200 vimefikiwa, hatua itakayochochea uzalishaji viwandani na kuongeza mnyororo wa thamani.

Aidha Dkt. Nchemba aliieleza timu hiyo kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza makubaliano Itifaki ya Fedha na Uwekezaji ya SADC ambapo Ibara ya tatu ya itifaki hiyo inazungumzia ushirikiano katika Muunganiko wa Uchumi Mpana (Macroeconomic Convergence).

Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Tathmini ya Uchumi kutoka SADC ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti wa Uchumi kutoka Benki ya Zimbabwe, Bw. Nebson Mupunga, alisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Itifaki ya Fedha na Uwekezaji lakini inahitaji kutatua changamoto zilizopo zikiwemo za nishati ili kuendelea kuimarisha Uchumi.

Akielezea madhumuni ya ziara ya kikazi ya timu hiyo, Bw. Mupunga alisema kuwa timu yake inafanya mapitio kwenye taarifa ya hali ya Uchumi ya Tanzania kwa mwaka 2023 na kuangalia utekelezaji wa mapendekezo ya Kisera ya Timu ya Wataalamu kutoka Afrika Kusini na Zimbabwe iliyofanyika mwaka 2016 na Eswatini na Msumbiji iliyofanyika mwaka 2020.

Timu ya wataalam wa SADC imekutatana na kufanya mazungumzo pia na wataalamu kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jumuiya ya Sekta Binafsi (TPSF), Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) na Economic and Social Research Foundation (ESRF)

Tanzania ilifanyiwa tathimini kama hii mwaka 2016 na 2020 na wataalamu kutoka nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe, Eswatini na Msumbiji mtawalia.

Share Story

Facebook Comments