Kampuni ya Kimataifa inayojihusisha na kufanya tathimini ya uwezo wa nchi kuyafikia masoko ya fedha ya kimataifa ya Moody’s Investors Limited, imepandisha daraja la nchi yetu kutoka B2 hadi B1. Kupanda huko kutokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Aidha, Moody’s imebadilisha mtazamo wa baadaye wa nchi kutoka chanya kuwa thabiti. Hii ni ishara nzuri ya imani katika uchumi wa Tanzania na uwezo wake wa kuhimili misukosuko mbalimbali ya kiuchumi. Kupandishwa katika daraja hili kutaongeza imani ya wawekezaji kuja Tanzania na kusaidia Serikali na mabenki ya ndani kupata mitaji kutoka kwenye masoko ya kimataifa kwa gharama nafuu zaidi.
Ikumbukwe kwamba mwezi Machi hadi Mei mwaka 2023, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza ilifanyiwa Tathmini ya Uwezo wa Nchi Kukopa na Kulipa madeni (Sovereign Credit Rating) na Kampuni ya Moody’s Investors na Fitch Ratings ambapo Kampuni ya Moody’s Investors iliipatia Tanzania alama B2 na Fitch iliipatia nchi alama B+ na mtazamo thabiti.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), wakati wowote, atazungumza na vyombo vya habari kufafanua zaidi maana ya matokeo hayo ya tathimini kwa nchi yetu.
Facebook Comments