Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameongoza mkutano wa Benki ya Dunia wa Jukwaa la Tatu la Kanda ya Afrika Kundi la Kwanza kwa nchi za Kipato cha Kati uliolenga kujadili namna mashirika ya fedha ya kimataifa yanavyoweza kuongeza fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi za kipato cha kati ili ziweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika nchi zao itakayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.

Akifungua mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Mkutano huo, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa Dunia inakabiliwa na migogoro mingi na changamoto za maendeleo ya kiuchumi ambazo zinasababisha kutofikiwa kikamilifu kwa malengo ya maendeleo endelevu (SDGs).

Alisema kuwa kupungua kwa nafasi ya kifedha katika kushughulikia migogoro hiyo kunadhoofisha uwezo wa Serikali za nchi hizo kufadhili programu za kijamii, kuharakisha ufufuaji wa Uchumi na pia kuongeza madeni katika nchi hizo.

“Mizozo inayoendelea nchini Urusi na Ukraine, Mashariki ya Kati na baadhi ya nchi nyingine za Afrika imechochea kupanda kwa bei ya vyakula na kuwasukuma mamilioni ya watu kwenye uhaba wa chakula”, alisema Dkt. Nchemba.

Aidha Dkt. Nchemba aliishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake wa kuzijengea uwezo taasisi katika kuyafikia maendeleo endelevu lakini pia kufufua uchumi kutokana na changamoto mbalimbali zinazotokea Duniani.

Vilevile alisema kuwa kukabiliana na changamoto zinazoikumba dunia sio kazi rahisi kwa nchi moja, hivyo ameomba kuwa na nguvu ya pamoja katika Kanda na Bara la Afrika katika kutafuta utatuzi wa changamoto hizo.

Dkt. Nchemba ameishukuru Benki ya Dunia kwa kummwamini kuongoza kikao hicho kikubwa lakini pia amewashukuru viongozi mbalimbali waliotoa mada ambazo zimewafunbua macho kwa kuona fursa zilizopo katika kukuza una kuwezesha biashara na pia kuwa na majadiliano mazuri wakati wa mikutano ijayo ya majira ya kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) itakayofanyika mwezi Aprili, 2024 jijini Washington D.C nchini Marekani.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ilitoa misaada na mikopo nafuu yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni tatu kwa nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Alisema kuwa mwaka wa fedha uliopita Benki ya Dunia kupitia Mfuko wa IDA ilitoa dola bilioni 2.4 na kwamba kiwango cha misaada na mikopo hiyo imeendelea kuongezeka na miongoni mwa nchi zilizonufaika na mpango huo ni Tanzania, Kenya na Eswatini.

Aidha, Bi. Kwakwa amevitaja vipaumbele vya Benki hiyo kuwa ni pamoja na kuhakikisha nchi zitapata umeme wa uhakika, kuwa na maendeleo ya kidigitali, upatikanaji wa ajira, mapinduzi ya kiuchumi, kujenga uwezo kwa rasilimali watu na masuala ya elimu.

Baadhi ya Viongozi walioshiriki mkutano huo ni pamoja na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, Makamu wa Rais wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) Kanda ya Afrika, Bw. Sergio Pimenta, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, Bi. Anshula Kant, Mawaziri wa fedha na Mipango (Magavana) na wajumbe wengine.

Share Story

Facebook Comments