Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) na Waziri wa Fedha, Bajeti na Mipango ya Uchumi wa Burundi, Mhe. Audace Niyonzima, wamekutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Washington D.C, nchini Marekani, kando ya mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambapo wamejadiliana kuhusu ujenzi wa Mradi wa Kikanda wa Reli ya Kisasa (SGR) utakaozihusisha nchi tatu za Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (Uvinza-Musongati-Gitega-Bujumbura-Uvira), yenye urefu wa kilometa 2,000.

Mradi huo utakao kuwa na vipande 7 (7 lots) unatarajiwa kuwa kiungo muhimu cha kukuza biashara na uchumi kati ya nchi hizo tatu kwa kuimarisha usafiri wa abiria na mizigo itakayotoka na kuingia katika nchi hizo huku Bandari ya Dar es Salaam ikitarajiwa kuwa kitovu cha biashara.

Hivi karibuni Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ilitoa dola milioni 91.76 (shilingi bilioni 231.3) kwa ajili ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha sita (Lot 6) na Saba (Lot 7) kitakachoiunganisha Tanzania na Burundi kutoka Malagarasi hadi Musongati chenye urefu wa kilomita 84 na baadae kuinganisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzia Malagarasi.

Share Story

Facebook Comments