Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Soko Kuu la Jiji la Mwanza, wenye thamani ya shilingi bilioni 23.4, Mradi ambão utakapo kamilika, utawezesha wafanyabiashara wapatao 1,400 kupata maeneo mazuri ya kufanyia biashara.

Aidha, mradi huo utakuwa na Maduka 514 (madogo, ya kati na makubwa) ndani na nje ya jengo, Vizimba 332 vya matunda na mbogamboga, Vizimba 372 vya nafaka, Mama lishe maeneo 12, eneo kwa ajili ya Wafanyabiashara ndogondogo (Machinga 167), ofisi 5, eneo moja la kukusanyia taka, eneo la maegesho ya Magari madogo 192 chini ya usawa wa Ardhi (basement) na vyoo.

Dkt. Nchemba alielezwa kuwa, mradi huu utasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji ambapo jumla ya Shillingi Billion 3.5 zinatarajiwa kukusanywa kwa mwaka, kupendezesha Jiji la Mwanza na kulifanya kuwa la Kisasa zaidi. Pia mradi huo utasaidia kukua kwa biashara nyingine kutoka kwa Wafanyabiashara wa ndani, mikoa ya jirani na nje ya nchi. Mradi huu umetoa ajira kwa vijana wapatao 175 ambao walikuwa wakiendelea na kazi mbalimbali za ujenzi.

Mhe. Dkt. Nchemba, yuko katika ziara ya siku 7 ya kikazi mkoani Mwanza, ambapo naungana na Mawaziri wenzake wa sekta mbalimbali wanaotembelea maeneo mbalimbali ya nchi, kutembelea, kukagua, kuweka mawe ya msingi na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika mikoa hiyo kwa manufaa ya wananchi kufuatia juhudi kubwa zilizofanywa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupeleka fedha nyingi za miradi katika mikoa yote nchini, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.

Share Story

Facebook Comments