Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amelishukuru Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa kupitia misaada na mikopo nafuu inayoipatia Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Dkt. Nchemba alitoa shukrani hizo Jijini Dodoma, wakati akifungua vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Timu ya Wataalam kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), iliyowasili nchini kufanya Tathimini ya Awamu ya Nne ya utekelezaji wa Program ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii pamoja na Awamu ya kwanza ya Programu ya Resilient and Sustainable Fund (RSF) ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema kuwa Tanzania inatekeleza Program ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia Programu hiyo ya Resilient and Sustainable Fund (RSF) baada ya kukidhi vigezo kufuatia uongozi bora wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa masuala ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
‘‘Baada ya kutekeleza kwa mafanikio programu nyingine zilizopita ikiwepo ile ya Dirisha la Dharura ambapo tulipata fedha za kukabiliana na athari za UVIKO-19 (Rapid Credit Facility- (RCF)), na huu wa ECF unalolenga kufufua na kuimarisha uchumi, Tanzania imetimiza sifa ya kutekeleza program ya RSF ambapo tutapata fedha za kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kutoka IMF,’’ alisema Dkt. Nchemba.
Alifafanua kuwa Timu za Wataalam wa pande hizo mbili zitakutana na kujadiliana zaidi kuhusu utekelezaji wa Program hizo na masuala yatakayokubalika wakati wa tathimini yatawasilishwa kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya IMF kwa ajili ya uidhinishwaji na kupata fedha.
Kwa upande wake Kiongozi wa Timu ya Wataalamu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Bw. Charalambos Tsangarides, alisema kuwa Shirika hilo limeridhishwa na utekelezaji wa programu ya ECF ambayo utekelezaji wake utakamilika katika mwaka wa fedha 2025/2026 na kuipongeza Tanzania kwa kupata idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo kutekeleza program ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Alisema kuwa Shirika lilo limeridhishwa na maendeleo mazuri kuhusu vigezo vya utendaji kazi wa programu ya ECF ambapo litapitia taarifa ya utekelezaji wake wakati wa tathmini.
Facebook Comments